Matatizo yanayowakumba watafsiri
Kan dea ɛfa Arthur Buliva ho nyina
Mtafsiri hana budi kuunda uswahiba na kamusi. Kamusi ni dafina muhimu sana kwa mtafsiri yeyote. Dola zinazoshughulikia ukuzaji wa kiswahili zimepiga hatua kubwa katika mawanda ya tafsiri kwa kuandika kamusi zenye istilahi anuwai. Mathalan, kamusi ya sheria, kamusi ya sheria, ya biashara, ya tiba, ya isimu.
Hivyo, mtafsiri mwenye ukakamavu hana kisingizio cha 'ufinyu' katika kazi yake. Ana bahari pana ya kuteka msamiati yake ili kukimu mahitaji yake kwa hadhira, wasikilizaji au wasomaji wake.
Licha ya ufanisi mkubwa uliopatikana katika nyanja ya taaluma za habari, kuna matatizo ambayo huwakumba watafsiri. Moja yazo ni kuwa tafsiri bado haijatambuliwa kama fani au taaluma maaluum.
Watafsiri wamepigwa chechele au kusahaulika katika dhima ya uandishi wa habari humu nchini. Kile kinachonifanya kusema hivyo ni kuwa chama cha waandishi wa habari kinaposambaza fomu za viingilio vya mwandishi bora nchini, huwa kuna viwango mbalimbali, japo huwezi kusoma kitengo cha watafsiri. Si hayo tu bali malipo ya watafsiri huwa ni duni.
Pengine mmoja aajiriwe na mashirika ya kimataifa, mshahara wako huwa ni wa kijungu jiko.
Tatizo lingine ni a ukosefu wa masomo kwa ujumla. Hakuna chuo ambacho kimejikita na kumakinika kufunza tafsiri nchini. Masomo ya tafsiri katika vyuo vya humu nchini ni ya kubabaisha. Hali hii ndiyo inayochangia kila mtafsiri kuibuka na maneno yake haja inapotokea. Masomo ya tafsiri yangewaongezea ujuzi wa kuchapa kazi zao kwa ufanisi mkubwa. Masomo yale yafungamanishwe na utamaduni, sayansi, uhusiano wa kimataifa na kadhalika.
Aidha, kuna tatizo la kuchipuka kwa uvumbuzi mpya katika mawanda ya sayansi na teknolojia. Anapokumbana na maneno mapya, mtafsiri hujipata akiwa tapa. Iwapo watafsiri wangebuni chama chao cha watafsiri kwa kushirikisha watafsiri wa mashirika mengine ya habari, wangetatua matatizo kama hayo yanayowakabili.
Kupiga hatua, basi ni kushirikiana katika safari hii ndefu yenye milima na mabonde ya kukikuza na kukieneza Kiswahili kulihali.
*Imenukuliwa kutoka Taifa Leo, Jumatano Julai 2, 2008
ReviewedCiteMatatizo yanayowakumba watafsiri. . In Essays. Retrieved 11:19 AM November 21st, 2008, from http://kasahorow.com/ak/content/matatizo_yanayowakumba_watafsiri
